Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) –ABNA– taarifa hiyo imesema kuwa, Taliban sasa imekaribia zaidi kuliko wakati wowote ule kufanikisha maono yake ya jamii inayowaondoa wanawake kabisa katika maisha ya umma. Mgogoro mkubwa zaidi wa haki za wanawake duniani una hatari ya kuonekana kuwa jambo la kawaida.
Umoja wa Mataifa umeeleza baadhi ya vizuizi vinavyowakabili wanawake nchini humo: wasichana wanazuiwa kuendelea na masomo baada ya kufikia umri wa miaka 13; wanawake wameondolewa kwenye ajira nyingi na kushiriki katika maisha ya kisiasa; na katika maeneo mengi ya nchi hawawezi kutembea barabarani bila kuandamana na mwanaume.
Taarifa hiyo pia imegusia ukosefu wa upatikanaji wa huduma bora za afya na matibabu, ongezeko la vifo vya wanawake na akina mama wajawazito, pamoja na kuongezeka kwa ukatili dhidi yao. Imebainishwa kuwa hali ya haki za wanawake nchini Afghanistan imeifanya nchi hiyo kushika nafasi ya pili duniani kwa pengo kubwa zaidi la kijinsia. Migogoro ya kibinadamu na umasikini wa kupindukia vimezidisha ugumu wa maisha kwa wote, hasa wanawake na wasichana.
Mwisho wa taarifa hiyo, kitengo cha wanawake cha Umoja wa Mataifa kimeutaka ulimwengu kuchukua hatua kwa ajili ya wanawake wa Afghanistan, na kutoa msaada wa kifedha na kiroho ili kujenga kizazi bora na mustakabali wenye mwanga zaidi nchini humo.
Your Comment